WAATHIRIKA wa mvua ya mawe na upepo mkali iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 40 katika kijiji cha Mwakata wilayani Kahama, Shinyanga, jana walitawanywa kwa mabomu ya machozi na polisi wa kutuliza ghasia (FFU) baada ya kufunga barabara kuu ya Isaka-Kahama kuelekea nchi jirani za Rwanda, Uganda na Burundi, kwa kulala barabarani na kuweka mawe na miti.
Tukio hilo lililotokea aljajiri jana liliathiri baadhi ya wasafiri wa mabasi makubwa yaliyokuwa yakisafiri kwenda mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma na mikoa ya jirani.
Waathirika hao walichukua uamuzi huo baada ya misaada ya chakula, magodoro, mablanketi na maturubai uliotolewa na wasamaria wema, ukiwa umefungiwa ndani ya darasa na wahusika wakishindwa kutimiza agizo la Waziri Mkuu Mizengo Pinda la kuwataka kuwapa msaada huo.
Akizungumza na Blogu hii, mwathirika wa tukio hilo, Benjamini Ndege, alisema wananchi waliamua kuchukua hatua hiyo ya kufunga barabara kutokana na kutojaliwa na serikali.
“Hawa waliofanya hivi ni wale ambao nyumba zao zimeharibika upande, zikiwa na mifugo na mali nyingine, lakini tunashindwa kuhudumiwa mahitaji muhimu…wanataka wote tukusanyike shuleni, sasa tunakaa hapo na mifugo yetu,” alihoji Ndege.
Ndege alisshangazwa na hatua ya mkuu wa wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, kutumia polisi kuvurumisha mabomu wakati wakiwa katika majonzi ya kupoteza ndugu zao katika janga hilo.
Alisema mabomu yalirushwa na polisi hao, yamesababisha akinamama na watoto kukimbilia porini wakihofia maisha yao kutokana na kutowahi kuona hali hiyo.
Naye Salome Maganga wa kijiji cha Mwakata, alisema wanahitaji msaada walioahidiwa wapatiwe kwani hakuna wanachotegemeza zaidi ya serikali kuwatendea yale waliyowaahidi.
“Tumeahidiwa msaada mbalimbali, lakini hatupewi na mvua inanyesha tunabaki kulowa nje wakati maturubai yapo…tunaomba tufanyiwe yale aliyoahidi Waziri Mkuu,” alisema Maganga.
Alisema wameandamana na kufunga barabara kwa lengo la kuishinikiza serikali kuwapatia misaada husika.
DC MPESYA
Hata hivyo, licha ya vurugu hizo kudumu kwa saa moja na nusu, lakini waathirika hao walionekana kumkataa mkuu wa wilaya hiyo, Benson Mpesya kuwapo eneo hilo na kumtaka aondoke kutokana na kudaiwa kuamuru polisi kuwavurumishia mabomu.

Akizungumzia tukio hilo, Mpesya alisema vitendo vilivyofanywa vya kufunga barabara vilihamasishwa na viongozi wa kisiasa wanaonekana kuingilia mchakato wa ugawaji chakula cha msaada.
“Hii yote ni hawa viongozi wa kisiasa wanaoingilia mchakato huu, kama hawanitaki watafute njia nyingine na wala si kupitia hali hii ya msaada,” alisema Mpesya.
Mpesya alisema wananchi wote walioathirika na janga hilo, walipewa chakula cha siku tatu tangu juzi, na leo (jana), tunawapa magodoro, maturubai na mablanketi kupitia viongozi wao wa vijiji.
Alisema chakula tani 20 toka ghara kuu la chakula Shinyanga, kinatarajiwa kuwasili wakati wowote kutokana na agizo la Waziri Mkuu, Pinda.
OCD Kahama
Akizungumzia maandamano yaliyofanywa na waathirika hao, mkuu wa polisi wilaya ya Kahama, Leonard Nyandahu, alisema wanafuatilia ili kufahamu tatizo la wananchi hao kuandamana.
“Lazima wananchi watii sheria bila shuruti, hivi sasa kuna watu wanne tunawachunguza na pale watakapobainika tunawachukulia hatua za kisheria,” alisema OCD Nyandahu.
MBUNGE MAIGE
Naye mbunge wa jimbo la Msalala, Ezekiel Maige, alisema viongozi wa serikali wanashindwa kutimiza wajibu wao kwa waathirika hao na kuamua kuwaangushia lawama wanasiasa.
“Wao ndiyo wanaozusha mgogoro huu, wananchi wanaambiwa na mkuu wa wilaya, chakula na vifaa vingine vipo vya kutosha, lakini hawavioni, sasa hapo nani wa kulaumiwa kama si wao…wanasiasa hawajeleta mvua hii lakini kikubwa ni kila mmoja kutimiza wajibu wake si kulaumiana,” alisema Maige.
Alisema kama misaada ipo kwa ajili yao, lazima viongozi wa serikali waitoe na kuwakabidhi wahusika wote waliokumbwa na janga hilo la mvua ya mawe na upepo mkali.
RC SHINYANGA
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Allynassoro Rufunga, alisema hali kwa waathirika wote inarejea kuwa vizuri kutokana na kukabidhiwa vifaa vyote husika vilivyotokana na msaada wa wasamaria wema.

Rufunga alisema serikali ya mkoa imetoa Sh.laki 3 kwa kila kaya kati ya 14 zilizofiwa kufuatia janga hilo lililotokea Jumanne usiku ikiwa ni rambirambi ili ziweze kuwasaidia kipindi hiki cha majonzi.
Alisema pesa hizo ni kati ya Sh.milioni 10 zilizotolewa na ofisi ya waziri mkuu ili kusaidia tukio hilo.
Hata hivyo, alisema misaada inayotolewa sasa kwa waathirika hao ni ile iliyotolewa na watu binafsi, taasisi zisizo za kiserikali na za kidini huku wakitakiwa kusubiri msaada wa serikali wakati wowote.
Aidha, Rufunga aliwaonya vijana wanaojiingiza kwa ajili ya kunufaika na misaada hiyo, kuacha mara moja tabia hiyo huku wakiwanyooshea kidole wananchi wa kijiji jirani cha Kagongwa kujiingiza katikati ya waathirika.
NAIBU WAZIRI AFYA
Akizungumza na baadhi ya waathirika wa janga hilo jana, Naibu waziri wa wizara ya afya, Kebwe Stephen, alisema wizara imetoa dawa zenye thamani ya Sh.milioni 47 kwa ajili ya kusaidia waathirika wa janga hilo.
Kwa mujibu wa serikali, mvua hiyo ilisababisha vifo vya watu 42 na majeruhi 92


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni