TMF, UN NA VYETI KWA WANAHABARI WAANDISHI WA DAWA ZA KULEVYA
SERIKALI
imesema inaandaa mswada wa sheria ambayo itawalinda watoaji wa taarifa
za masuala ya uhalifu ikiwa ni jitihada za kuimarisha mapambano dhidi ya
vitendo mbalimbali vya uhalifu nchini Tanzania. Kauli hiyo ilitolewa
mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Bw. George Masaju alipokuwa akitoa vyeti kwa baadhi ya waandishi wa
habari waliokuwa katika mpango wa kuandika habari za dawa za kulevya
pamoja na mafanikio na changamoto za mpango wa milenia.
Akizungumza
katika hafla hiyo iliyoandaliwa kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa
(UN) na Mfuko wa Wanahabari Tanzania (TMF), Masaju alisema kwa sasa ni
Sheria ya Makosa ya Rushwa (ufisadi) tu ndiyo inayowalinda watoaji wa
taarifa hizo kwani imekataza wao kutajwa tofauti katika maeneo mengine
ya sheria.
Alisema katika sheria hiyo mpya
inayokusudiwa kutungwa na Serikali itapanua wigo wa ulinzi kwa watoaji
wa taarifa kutotajwa endapo watatoa taarifa juu ya makosa yoyote jambo
ambalo alisema litasaidia katika mapambano ya uhalifu. "Serikali
inaandaa muswada wa Sheria ya kuwalinda watoa taarifa wa vitendo vya
uhalifu (whistle blowers protection bill) ili kuimarisha mapambano dhidi
ya uhalifu wa aina zozote nchini. Kwa sasa ni watoa taarifa wa makosa
ya rushwa (ufisadi) tu ndio wanatamkwa katika sheria ya kuzuia na
Kupambana na Rushwa, 2007 kulindwa wasitajwe," alisema Mwanasheria Mkuu.
Aidha
alisema Sheria mpya ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ya Mwaka
2015 ambayo imepitishwa na Bunge hivi karibuni imetungwa kwa kuzingatia
mapungufu ya sheria za nyuma hivyo itakuwa na nguvu zaidi ya kupambana
na uhalifu huo tofauti na ilivyokuwa awali.
Alikiri
kuwa sheria ya awali ilikuwa na mapungufu kadhaa jambo ambalo
lilichangia sheria hiyo kushindwa kufanya kazi kikamilifu katika
mapambano. Alisema miongozi mwa mapungufu kwa sheria iliyokuwa ikitumika
awali ni pamoja na kutotoa adhabu kulingana na ukubwa wa kosa, na
haikuainisha masharti bora ya udhibiti wa madawa ya kulevya kama ilivyo
kwa sheria mpya.
Alisema sheria mpya imeanzisha
Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya ambapo mwenyekiti wake ni
Waziri Mkuu wa Tanzania na wajumbe wake watatoka pande zote za Muungano
yaani Tanzania Bara na Visiwani, alisema kazi kubwa ya balaza hilo ni
kusimamia utekelezaji wa Sera ya Udhibiti wa Dawa za kulevya.
"Sheria
iliyopo ina udhaifu wa adhabu, haitoi adhabu kulingana na ukubwa wa
kosa kwenye baadhi ya makosa, hivyo kusababisha kukosekana kwa mizania
ya haki. Sheria mpya imeweka kima cha kuanzia cha adhabu iwe ni faini au
kifungo. ...Mfano sheria mpya imeweka adhabu ya faini isiyopungua
milioni 50 na isiyozidi milioni 500 au kifungo kisichopungua miaka 7 na
kisichozidi miaka 30 au vyote kwa pamoja." Alifafanua Masaju katika
hotuba yake.













Hakuna maoni:
Chapisha Maoni